Translator

IMETOSHA

HHCTZ

BREAKING NEWS



BREAKING NEWS: Losam5 ....>>>>>>"Fashion,Entertainments,Science and Technology".......>>>>>>>Smile's Zone 5

Jumanne, 24 Desemba 2013

Je, Matibabu ya Kisasa Yanaweza Kufaulu?

WATU wengi hujifunza kutimiza mambo wasiyoweza kwa msaada wa wengine. Jambo sawa na hilo limetukia katika matibabu. Watafiti wa tiba wamefanya maendeleo makubwa kwa kujifunza na kusitawisha matibabu yaliyobuniwa na madaktari na wanatiba maarufu wa kale.

Wanaume mashuhuri kama vile Hippocrates na Pasteur, pamoja na wengine wasiojulikana sana kama Vesalius na William Morton ni baadhi ya madaktari mashuhuri waliokuwapo kale. Wanaume hao waliboreshaje matibabu ya kisasa?

Katika nyakati za kale mara nyingi matibabu hayakutegemea sayansi bali ushirikina na desturi za kidini.  Kitabu The Epic of Medicine, kilichohaririwa na Dakt. Felix Marti-Ibañez, chasema hivi: “Ili kupambana na magonjwa . . . , wakazi wa Mesopotamia walitumia imani za kidini katika matibabu, kwa sababu waliamini kwamba magonjwa ni adhabu kutoka kwa miungu.” Matibabu ya Misri yaliyoenea baadaye, pia yalitegemea dini. Kwa hiyo, tangu nyakati za kale, madaktari walisifiwa sana na watu wa dini.
Dakt. Thomas A. Preston asema hivi kwenye kitabu chake The Clay Pedestal: “Imani nyingi za watu wa kale zimeathiri sana matibabu ya leo. Kwa mfano, waliamini kwamba mgonjwa hawezi kuzuia ugonjwa wake. Na kwamba anaweza kutibiwa tu na daktari kwa nguvu za uchawi.”

Kuweka Misingi
Hata hivyo, baada ya muda matibabu yakazidi kuwa ya kisayansi. Hippocrates alikuwa daktari mashuhuri zaidi ya madaktari wote wa sayansi nyakati za kale. Alizaliwa wapata mwaka wa 460 K.W.K., kwenye kisiwa cha Kos huko Ugiriki. Watu wengi humwona kuwa mwanzilishi wa matibabu huko Ulaya. Hippocrates alianzisha matibabu ambayo yalitegemea elimu. Alipinga wazo la kwamba magonjwa yalikuwa adhabu kutoka kwa mungu na kusisitiza kwamba magonjwa husababishwa na hali za asili. Kwa mfano, kwa miaka mingi ugonjwa wa kifafa uliitwa ugonjwa mtakatifu kwa sababu ya imani ya kwamba ungeweza kutibiwa na miungu tu. Lakini Hippocrates akaandika hivi: “Mimi sidhani ule unaoitwa ugonjwa Mtakatifu huletwa na miungu au ni mtakatifu kuliko magonjwa mengine, bali naamini kwamba unasababishwa na hali fulani ya asili.” Hippocrates alikuwa pia daktari wa kwanza kabisa kuchunguza dalili za magonjwa mbalimbali na kuziandika ili zitumiwe baadaye kwa matibabu.

Karne nyingi baadaye, Galen, daktari Mgiriki aliyezaliwa mwaka wa 129 W.K., alifanya pia utafiti wa kisayansi wa hali ya juu. Galen alipasua na kuchunguza miili ya wanadamu na wanyama, kisha akaandika kitabu kuhusu maumbile ya mwili. Kitabu hicho kilitumiwa na madaktari kwa karne nyingi! Andreas Vesalius, aliyezaliwa huko Brussels mnamo mwaka wa 1514, aliandika kitabu On the Structure of the Human Body. Kitabu hicho kilichambuliwa na watu kwa sababu kilipinga mambo mengi yaliyoandikwa na Galen, lakini kiliweka msingi wa elimu ya kisasa ya maumbile ya mwili. Kitabu Die Grossen (Watu Maarufu), chasema kwamba Vesalius alipata kuwa “mmojawapo wa watafiti muhimu sana wa kitiba wasio na kifani.”

Baada ya muda nadharia za Galen kuhusu moyo na mzunguko wa damu zilibadilishwa kabisa.* Daktari Mwingereza William Harvey alipasua na kuchunguza miili ya wanyama na ndege kwa miaka mingi. Alichunguza utendaji wa vali za moyo, akapima kiasi cha damu katika vyumba vyote moyoni, na akakadiria kiasi cha damu mwilini. Mwaka wa 1628, Harvey alichapisha uchunguzi wake katika kitabu On the Motion of the Heart and Blood in Animals. Alichambuliwa, alipingwa, alishambuliwa, na hata kutukanwa. Lakini uchunguzi wake ulileta maendeleo muhimu sana ya kitiba. Aligundua mfumo wa mzunguko wa damu mwilini!

Vinyozi Wanakuwa Wapasuaji
Maendeleo makubwa yalikuwa yakifanywa pia katika upasuaji. Katika Enzi za Kati, nyakati nyingine upasuaji ulifanywa na vinyozi. Si ajabu, watu fulani husema kwamba mwanzilishi wa upasuaji wa kisasa alikuwa Mfaransa aliyeitwa Ambroise Paré aliyeishi katika karne ya 16 na alitumikia wafalme wanne wa Ufaransa. Paré alibuni pia vifaa kadhaa vya upasuaji.

Mojawapo ya matatizo makubwa yaliyowasumbua wapasuaji katika karne ya 19 ni kutoweza kupunguza maumivu wakati wa upasuaji. Lakini katika mwaka wa 1846, daktari wa meno anayeitwa William Morton alianzisha mbinu za unusukaputi katika upasuaji.*

Mnamo mwaka wa 1895, mwanafizikia Mjerumani Wilhelm Röntgen aliona miale ikipenya nyama lakini si mifupa alipokuwa akifanya majaribio kwa kutumia umeme. Hakujua chanzo cha miale hiyo, kwa hiyo akaiita miale x (miale isiyojulikana) au eksirei. Kulingana na kitabu Die Großen Deutschen (Wajerumani Maarufu), Röntgen alimwambia hivi mkewe: “Watu watasema: ‘Röntgen ana kichaa.’” Watu fulani walisema hivyo. Lakini uvumbuzi wake uliboresha upasuaji. Sasa madaktari-wapasuaji wangeweza kuchunguza ndani ya mwili bila upasuaji.

Kushinda Magonjwa
Kwa miaka mingi magonjwa ya kuambukiza kama vile ndui yalienea kasi, yalitisha na kuangamiza watu wengi. Ar-Rāzī, Mwajemi wa karne ya tisa ambaye wakati huo alionwa na baadhi ya watu kuwa daktari mashuhuri zaidi katika nchi za Kiislamu, aliandika ufafanuzi wa kwanza sahihi wa kitiba kuhusu ugonjwa wa ndui. Lakini dawa ya kutibu ndui ilivumbuliwa karne nyingi baadaye na daktari Mwingereza aitwaye Edward Jenner. Jenner alisema kwamba mtu akishikwa na ndui ya ng’ombe (cowpox)—ugonjwa usiodhuru—basi hawezi kuambukizwa ndui (smallpox) tena. Kwa kutegemea uchunguzi huo, Jenner alitumia viini vya ndui ya ng’ombe kutengeneza chanjo ya ndui. Alifanya hivyo mwaka wa 1796. Jenner alichambuliwa na kupingwa kama wavumbuzi wengine waliomtangulia. Lakini hatimaye uvumbuzi huo wa chanjo ulisaidia kukomesha ugonjwa huo na ukatokeza njia mpya ya matibabu.

Mfaransa aitwaye Louis Pasteur alitumia chanjo kupambana na kichaa cha mbwa na maradhi ya mifugo (anthrax). Alithibitisha pia kwamba magonjwa husababishwa na viini. Mwaka wa 1882, Robert Koch aligundua viini vinavyosababisha kifua kikuu. Mwanahistoria mmoja aliuita ugonjwa huo “ugonjwa unaoua watu wengi zaidi katika karne ya kumi na tisa.” Mwaka mmoja hivi baadaye, Koch aligundua viini vinavyosababisha kipindupindu. Gazeti Life lasema hivi: “Kazi ya Pasteur na Koch ilianzisha sayansi ya kuchunguza viini na ikaboresha elimu ya kinga-maradhi, usafi na afya. Uvumbuzi huo umerefusha muda wa maisha ya mwanadamu kuliko maendeleo mengineyo yote ya kisayansi ya muda wa miaka 1,000 iliyopita.”

Matibabu Katika Karne ya Ishirini
Mwanzoni mwa karne ya 20, matibabu yalitegemea mavumbuzi ya matabibu hao wenye akili na wengineo. Tangu hapo, kumekuwa na maendeleo makubwa sana ya kitiba. Wamebuni insulini ya kupambana na ugonjwa wa sukari, tiba ya kemikali kwa ajili ya kansa, homoni za kutibu magonjwa ya tezi, viuavijasumu vinavyotibu kifua kikuu, klorokwini inayotibu aina fulani za malaria na usafishaji wa damu kwa mashine ili kutibu matatizo ya figo, vilevile wamefanya upasuaji wa moyo, na upachikaji wa viungo vya mwili na matibabu mengine mengi.

Lakini sasa tukiwa mwanzoni mwa karne ya 21, je, tiba itaandaa “kiwango kinachokubalika cha afya kwa watu wote ulimwenguni”?